Simba imeitisha mkutano mkuu wa dharura klabuni Msimbazi jijini Dar es Salaam leo kupinga maamuzi yaliyotolewa na TFF jana baada ya Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya shirikisho hilo la soka nchini kumuidhinisha beki wao wa zamani Kelvin Yondani kuichezea Yanga.
Kamati hiyo iliyo chini ya mwenyekiti wake, Alex Mgongolwa, jana pia ilimuidhinisha kiungo wa zamani wa Azam, Ramadhani Chombo 'Redondo' kuchezea Simba huku ikiipa Yanga siku 21 kuwalipa Simba Dola za Marekani 32,000 ambazo beki wake mpya Mbuyu Twite alikiri kupokea kutoka katika klabu hiyo ambayo nayo ilikuwa na nia ya kumsajili kabla ya kubadili mawazo na kutua kwa wapinzani wao.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, alisema jana kuwa wameitisha mkutano mkuu wa dharura utakaofanyika leo jioni kwenye makao makuu ya klabu hiyo kupinga maamuzi yaliyotolewa na Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji kwamba hayakufuata kanuni.
Rage alisema kuwa agenda ya mkutano mkuu huo wa leo itakuwa ni moja ya kutaka ridhaa ya wanachama juu ya timu yao kuendelea kushiriki au kujitoa katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara itakayofanyika kuanzia Jumamosi.
Alisema haiwezekani kamati hiyo ambaye yeye pia ni mjumbe ipitishe maamuzi kwa kupiga kura na hawakusubiri uchunguzi wa saini za mchezaji huyo ambaye awali alidaiwa kusaini mkataba mpya wa kuichezea Simba kabla ya kutimkia Yanga kama ilivyopendekezwa.
Akizungumza jana, Mgongolwa alisema kuwa kamati yake imebaini kwamba Yanga ilifuata taratibu zote katika kumsajili Twite kama kanuni ya Uhamisho ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) 18(3) inavyoeleza.
Alisema pia kamati imemuidhinisha Yondani kuichezea Yanga kwa mujibu wa ibara ya 44(3) ya Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za TFF kwa kuwa klabu hiyo ya Jangwani ilifuata taratibu zote katika kumsajili hivyo ni mchezaji wake halali.
Aliongeza kuwa kutokana na madai ya Simba kuhusu mchezaji huyo alisaini mkataba na klabu yao, Wekundu wa Msimbazi
wametakiwa kupitia katika mamlaka nyingine (Polisi) ili kuthibitisha hilo na baada ya uthibitisho iwasilishe malalamiko yake kwenye Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji au mamlaka zozote za kisheria kwa mujibu wa madai/lalamiko yao.
Alisema kamati yake pia imeyatupa mapingamizi ya Yanga dhidi ya wachezaji waliotemwa na klabu ya Simba wakati walisajiliwa kuicheza timu hiyo katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki (Kombe la Kagame) kwa sababu hakukuwa na malalamiko yoyote kutoka kwa wachezaji hao ambao ni Dan Mrwanda, Haruna Shamte, Kanu Mbiavanga na Lino Masombo.
Pia kamati hiyo ilisema kuwa Mussa Hassan 'Mgosi' aliyesajiliwa na JKT Ruvu hataweza kuichezea timu hiyo mpaka hati yake ya uhamisho (ITC) kutoka DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo itakapowasili sawa na Ayoub Isiko wa Mtibwa Sugar atakapopata ITC kutoka Bull ya Uganda.
Hata hivyo, kamati hiyo iliamua kuwa Enyima Ariwodo ni mchezaji halali wa Kagera Sugar kwa vile Toto Africans ilishindwa kutimiza masharti ya mkataba wake.
Alisema Redondo ameidhinishwa kuchezea Simba kwa kuzingatia mchezo wa haki na uungwana baada ya klabu hiyo na Azam kufikia makubaliano kuhusu mchezaji huyo.
Mgongolwa aliongeza kuwa Yanga imetakiwa kuilipa Kagera Sugar ada ya uhamisho ya Sh. milioni 5 ndani ya siku 21 kuanzia juzi na Simba imepewa siku 21 kuanzia Septemba 10 mwaka huu iwe imeilipa Super Falcon fedha za matunzo ya Edward Christopher aliyesajiliwa katika klabu hiyo pamoja na Rollingstone ambao walimtunza Kigi Makasy.
Alisema Azam nao wamepewa siku 21 kuilipa Flamingo fedha za kuvunja mkataba wa kumsajili Kelvin Friday wakati African Lyon wametakiwa kulipa Sh. milioni moja kutokana na kumsaini mchezaji wa Super Falcon, Robert Joseph Mkhotya.
chanzo:nipashe
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment