Pages

Monday, 12 November 2012

Simba kimenuka tena



WAKATI mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania bara, Simba jana wakipokea kichapo cha pili mfululizo, Kocha Mkuu, Milovan Cirkovic amevunja ukimya na kuulalamika uongozi kutomshirikisha katika maamuzi yaliyomng’oa kikosini beki Juma Nyoso.
Akizungumza baada ya pambano hilo, Milovan aliutupia lawama uongozi wa Simba kwa kumshusha Nyoso bila kumshirikisha na kuchangia kuidhoofisha safu ya ulinzi na timu kwa ujumla, huku akikiri wazi kudhihiri kwa pengo la mlinda mlango wake, Juma Kaseja.
Kauli ya Milovan na misimamo wa mashabiki, umezua hali ya sintofahamu klabuni, ambapo mabango ya kumtaka Geofrey Nyange ‘Kaburu’ kuachia ngazi yalionekana, ambapo mashabiki wa tawi la Simba Vuvuzela, walionesha bango lililoandikwa ‘Simba bila Kaburu inawezekana.’
Ndani ya uwanja, Simba kama ilivyokuwa kwa washindi wa pili wa msimu uliopita Azam FC, kwa pamoja zimeshindwa kuing’oa Yanga katika kilele cha ligi hiyo, baada ya zote kujikuta zikipokea vichapo kwenye viwanja vya Taifa jijini Dar es Salaam na Mkwakwani jijini Tanga.
Katika mechi hizo za kukamilisha mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 14, Simba imeendeleza matokeo mabovu, safari hii ikiwa Uwanja wa Taifa, baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Toto Africans, huku Azam ikichapwa mabao 2-1 na Mgambo JKT ya Handeni.
Simba iliingia uwanjani ikiwa nafasi ya tatu ya msimamo wa ligi kwa pointi zao 23, moja nyuma ya Azam iliyoingia dimbani ikiwa nafasi ya pili kwa pointi 24 – zote zikipania ushindi ili kuing’oa Yanga iliyokaa kileleni ikiwa na pointi 26.
Jijini Dar es Salaam, pambano lilianza kwa kasi na mashambulizi ya hapa na pale, ambapo Nassor Masoud ‘Cholo’ alionywa kwa kadi ya njano mapema dakika ya nane, kutokana na rafu yake kwa mchezaji wa Toto wakati wakiwania mpira.
Dakika ya 11, Amri Kiemba alishindwa kuipa Simba bao baada ya shuti yake kudakwa na kipa Erick Ngwengwe, wakati dakika ya 24, Felix Sunzu nae alikosa bao baada ya mpira wake wa kichwa kugonga mwamba na kudakwa na kipa huyo.
Simba ilizidi kushambulia lango la Toto na kiungo Mussa Said alifanya kazi ya ziada katika dakika ya 40, alipookoa mpira uliopigwa na Kiemba, huku mlinda mlango Ngwengwe akiwa amepotea maboya.
Hadi filimbi ya mapumziko ya mwamuzi Judith Gamba wa Arusha, si Simba wala Toto waliofanikiwa kutikisa nyavu, licha ya Wekundu wa Msimbazi kushambulia mara kadhaa.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na mashambulizi ya kila upande, ambapo Mussa Said, aliipatia Toto bao katika dakika ya 73 kwa kichwa, akiunganisha mpira wa adhabu ndogo wa Mohammed Jingo.
Bao hilo lilipokelewa kwa shangwe na mashabiki wa Yanga, ambao licha ya upinzani wa jadi uliopo dhidi ya Simba, lakini pia ina undugu na Toto.
Kwa ushindi huo Toto imeongeza pointi zake kutoka tisa hadi 12, ingawa imesalia kwenye nafasi ya 12 baada ya Mgambo nao kuwachapa Azam.
Simba: William Mweta, Nassor Masoud ‘Cholo,’, Paul Ngalema, Komanbil Keita, Shomari Kapombe, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi na Mrisho Ngasa.
Toto: Erick Ngwengwe, Ally Ahmad, Erick Marilo, Everist Maganga, Peter Mutabuzi, Msafiri Hamisi, Mussa Saidi, Emmaanuel Swita, Kheri Mohammed, Selema Kibuta na Mohammed Jingo.
Kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, mabao mawili kutoka kwa Issa Kandulu na Nassor Gumbo, yalitosha kuipa pointi tatu muhimu Mgambo JKT, huku Kipre Tchetche akiifungia Azam bao la kufutia machozi na kudumisha mwendo wa kusuasua.
Licha ya jitihada za Azam kutaka kubadili hali ya mambo katika timu yao, Mgambo ikafanikiwa kuwazima kwa bao la Gumbo la dakika ya 78, akiyemalizia pasi ya kifua ya mfungaji wa bao la kwanza, Kandulu.
chanzo:daima

0 comments:

Post a Comment