Timu hiyo ya vijana ya Simba ilitwaa ubingwa wa Super8 baada ya kuinyuka Mtibwa mabao 4-3 na kujinyakulia kitita cha Sh40milioni.
Uongozi wa Simba kupitia kwa kocha wake, Selemani Matola, ulitangaza kutoa Sh1 milioni kwa kila mchezaji kama motisha ya wachezaji hao baada ya kutwaa Kombe la Super8 huku ikielezwa kuwa ni sehemu ya vijana wao kusherehekea Sikukuu ya Eid el Fitr.
Habari za uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo zinadai kuwa uongozi wa Simba umempa mhasibu wa klabu hiyo, Sh20milioni na mpaka sasa wachezaji hao hawajapatiwa fedha hizo.
"Wachezaji wanasumbua sana, mi nashangaa uongozi umetoa milioni 20 tu wakati wachezaji wapo 27 sasa hizo milioni 20 atapewa nan i atabaki?
"Hebu niambie, hao wachezaji saba watakaobaki watapewa nini? benchi la ufundi je tuseme halina kitu chochote?...wanachofanya sio kitu cha kistarabu kabisa wanakatisha tamaa hata hawa watoto," kilisema chanzo cha habari.
Habari zaidi ambazo Mwananchi imezipata zinasema kuwa mbali na hayo, wachezaji wa Mtibwa Sugar walipata Sh200,000 kila mchezaji kutokana na mapato ya geti wakati wachezaji Simba walipewa Sh40,000 ambazo zote hizo ni nje ya zawadi. Mtibwa ilipata Sh20mil kwa kushika nafasi ya pili.
Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Evodius Mtawala alipotafutwa jana alisema suala hilo liko juu yake na hata hivyo msemaji ni Ofisa Habari wa klabu, Ezekiel Kamwaga.
Kamwaga alipotafutwa alikiri kuwa ni kweli wachezaji hao hawajalipwa fedha hizo, na akasema kama klabu wanaandaa utaratibu wa malipo kwa wachezaji hao.
"Kuna wachezaji kama Shomari Kapombe alicheza mechi moja utamlipaje sawa na wachezaji waliocheza mechi zote, mambo yakikamilika watapewa fedha zao," alisema Kamwaga.
Wakati huo huo; Uongozi wa Simba umesema utakutana hivi karibuni kufanya mchujo wa wachezaji wa kigeni ili kupata watano kwa ajili ya Ligi Kuu na mechi za kimataifa.
Uamuzi huo wa Simba unakuja baada ya Shirikisho la soka Tanzania, TFF, kutoa orodha ya wachezaji walioombewa hati za uhamisho wa kimataifa, ITC kati yao akiwemo, Musa Mudde (Sofapaka, Kenya) na Daniel Akuffor kutoka Stella Abidjan, Ivory Coast.
Kamwaga alisema kuwa wachezaji wa kigeni wapo sita, lakini wao kama klabu wanajua ni lazima wa baki watano hivyo kabla ya Septemba 10 watakutana ili waweze kufanya mchujo.
"Tunaendesha ligi kwa kufuata kanuni ambayo inasema wachezaji wa kigeni mwisho watano hatuwezi kuipinga tutafanya mchujo kutoka miongoni mwa hao," alisema Kamwaga.
Kuhusu suala la Salum Kinje na Pascal Ochieng, Kamwaga alisema wapo katika hatua nzuri ya kupata ITC za wachezaji hao.
"Tuna matumaini ya kukamilisha suala hilo ndani ya saa 12 zijazo na hivi tunavyoongea kuna ujumbe wa Simba yuko jijini Nairobi nchini Kenya kufuatilia hati hizo," alisema Kamwaga.
chanzo:http://www.mwananchi.co.tz
Haya sasa! yameshakuwa hayo tena? Uongozi wa Simba uache kuwafanyia uhuni hao vijana vinginevyo itakuwa ni majuto tupu hapo baadae...
ReplyDelete