Pages

Thursday 6 September 2012

NIYONZIMA KUITOSA YANGA!!

KIUNGO wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Niyonzima amesema anatarajia kuachana na mabingwa wa Kombe la Kagame, Yanga mwishoni mwa msimu huu.

Akizungumza na gazeti la New Times la Rwanda, Niyonzima alisema anatarajia kwenda kucheza soka la kulipwa Ulaya, lakini kwa sasa anasubiri mkataba wake na Yanga umalizike mwezi Mei ili aondoke.
 
"Meneja wangu amekuwa akihangaika kunitafutia timu Ulaya. Tumekuwa na mawasiliano na klabu za ligi daraja la pili Hispania na Ligi Daraja la kwanza Ubelgiji.
 
"Kama mambo yakienda vizuri wakati wowote naweza kwenda kujiunga na timu hiyo (hakutaja jina la timu), kwa sababu mkataba wangu na Yanga unaniruhusu kuondoka kama nikipata klabu kubwa zaidi," aliongeza Niyonzima.

Katika hatua nyingine viwango vya hali ya juu vilivyoonyeshwa na chipukizi wa Yanga, Simon Msuva na Frank Domayo vimewaweka pabaya wakongwe Nizar Khalfan na Juma Seif ‘Kijiko’.

Kocha wa Yanga, Tom Saintfiet alisema jana amekuwa akifurahishwa na viwango ambavyo vimekuwa vikionyeshwa na chipukizi hao tangu walipojiunga na timu hiyo.

Mbelgiji huyo alisema,“nimekuwa nikimuanzisha Msuva badala ya Nizar nikiwa na lengo la kumjenga na kumpa uzoefu zaidi. Ni mchezaji anayekuja vizuri. Nafikiri atakuwa tegemeo kwa siku za baadaye.”

Msuva amecheza mechi zote tano za Yanga za kujipima ubavu kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu na kupachika mabao mawili dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda na African Lyon, pia alitoa pasi ya bao lililofungwa na Said Bahanunzi dhidi ya Coastal Union wakati Yanga ikishinda 2-1. 

Domayo alitua Yanga akitokea JKT Ruvu ya Pwani na mpaka ameonyesha uwezo mkubwa hata kumfanya Kijiko aliyetamba na klabu hiyo msimu uliopita kuwa chaguo la tatu.

Domayo amekuwa akiingizwa kipindi cha pili katika kikosi cha Yanga na kuonyesha kiwango kizuri.

Wakati huo huo; Kocha Saintfiet amewaambia wachezaji wake kwamba hakuna timu ndogo katika Ligi Kuu, hivyo wanatakiwa kutilia mkazo mchezo wao wa ufunguzi dhidi ya Prison. 
“Nafikiri mchezo utakuwa mgumu tofauti na wengi wanavyofikiri. Sijabahatika kuwaona Prisons wanavyocheza ni vigumu kupanga mbinu za kukabiliana nao,”alisema Saintfiet.

Alisema, “hatuna sababu ya kuidharau Prisons kwa sababu lengo letu kubwa ni kushinda kila mchezo na kuondoka na pointi tatu.”

Saintfiet alisema kuwa siku zote timu ndogo inavyocheza na timu kubwa huwa wachezaji wake wanapania na kuufanya mchezo huo kuwa mgumu.

“Tunacheza ugenini. Nafikiri litakuwa jambo zuri kwetu kama tutaanza na ushindi. Nimeongea na wachezaji wangu na nimewaambia tunatakiwa kuupa uzito mchezo huo,” alisema Saintfiet.

Katika hatua nyingine, beki Kelvin Yondan na kiungo, Nurdin Bakari walishindwa kushiriki mazoezi ya jana kutokana na kusumbuliwa na maradhi tofauti.

Daktari wa timu hiyo, Juma Sufian alisema jana kuwa Yondan anauguza majeraha ya kifundo cha mguu wakati Nurdin anasumbuliwa na ugonjwa wa malaria. 
chanzo:http://www.mwananchi.co.tz

0 comments:

Post a Comment