Pages

Thursday, 6 September 2012

SIMBA WATANDIKWA MABAO 3-0 NA SOFAPAKA!!!

MABINGWA wa Tanzania, Simba walishindwa kukonga nyoyo za mashabiki wao baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Sofapaka ya Kenya katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mabingwa hao wa zamani wa Kenya, Sofapaka walitalawa sehemu kubwa ya mchezo huo na kufanikiwa kupata mabao yao kupitia kwa John Baraza aliyefunga mabao mawili na Joseph Nyanga.

Matokeo hayo yameacha maswali mengi kwa Simba ambao ukuta wake chini ya mabeki wake wa kati Komabil Keita na Pascal Ochieng ulionekana kuyumba na kukosa mawasiliano. 

Sofapaka walianza mchezo kwa kasi na kufika langoni kwa Simba katika dakika ya 5 kupitia kwa mshambuliaji wake Joseph Nyanga ambaye alipiga shuti lakini lilitoka nje.

Dakika mbili baadaye beki mpya wa Simba, Komabil Keita alifanya kazi ya ziada kuokoa mpira uliokuwa ikielekea langoni mwao na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Simba walijibu mapigo dakika ya 8, ambapo Mrisho Ngassa aliwatoka mabeki wa Sofapaka na kupiga krosi, lakini Daniel Akuffo alishindwa kumalizia mpira na kuokolewa na mabeki.

Mshambuliaji Baraza aliwanyamazisha mashabiki wa Simba kwa kufunga bao la kuongoza kwa Sofapaka katika dakika ya 10 kwa mkwaju wa penalti baada ya beki Keita kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.
Akuffo alijitahidi kutafuta nafasi huku na kule, lakini mabeki wa Sofapaka wakiongozwa na nahodha James Situma na George Owino walikuwa makini kumdhibiti asifurukute.

Katika dakika ya 35, Simba walipata pigo baada ya Akuffo kugongana na beki wa Sofapaka na kuzimia kwa dakika kadhaa na kusababisha wachezaji wenzake kuvua jezi na kuanza kumpepea kabla ya kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Abdallah Juma.

Wakati mpira ukielekea mapumziko Edward Christopher alipoteza nafasi nzuri ya kuisawazisha Simba katika dakika ya 44 baada ya kuzubaa na kutoa mwanya kwa beki Edgar Ochieng kuuwahi mpira na kuupiga nje.

Simba walicheza vizuri katika dakika 45 za kwanza, lakini walinzi wake walikosa mawasiliano kwenye safu ya ulinzi kati ya Keita na Pascal Ochieng na kutoa mwanya kwa washambuliaji wa Sofapaka kulifikia kirahisi lango.

Kipindi cha pili Simba ilimpumzisha Salum Kinje na kumwingiza Ramadhan Chombo na kubadilisha mfumo hivyo kutumia 4-4-2 wakati Sofapaka wenyewe walitumia 4-5-1.

Mshambuliaji Baraza aliendelea kuwa mwiba kwa ngome ya Simba kwani katika dakika ya 57 aliipatia Sofapaka bao la pili kwa kumwinulia mpira juu 'kumning'iniza' kipa Juma Kaseja na kufunga bao hilo.

Sofapaka iliendelea machungu kwa mamia ya mashabiki wa Simba walijitokeza kukitazama kikosi chao kwa mara ya kwanza baada ya kurejea kutoka kambini mkoani Arusha kwa kupata bao la tatu dakika ya 66 lililofungwa na Nyanga akiunganisha vizuri pasi ya  Felly Malumba.

Kocha wa Simba Milovan Cirkovic aliwapumzisha Ochieng, Amir Maftah, Edward na Keita na kuwaingiza Kigi Makassi, Juma Nyoso, Saidi Nassor na Paul Ngalema mabadiliko ambayo hayakuisaidia timu hiyo.
chanzohttp://www.mwananchi.co.tz:

0 comments:

Post a Comment