Wafungaji bora Afrika Mashariki na Kati, Said Bahanunzi na Hamisi Kiiza kucheza mechi mbili bila kupata bao na safu ya ulinzi iliyodhaniwa kuwa mbovu ya Simba kutoruhusu goli hata moja ni miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa gumzo kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara iliyoanza Jumamosi iliyopita Septemba 15.
Mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Yanga kushidwa kushinda mechi hata moja kati ya mbili walizocheza na kushika nafasi ya 13 mpaka sasa ni mambo ambayo yamewashangaza mashabiki wengi wa soka nchini.
Yanga iliyopewa nafasi kubwa kufanya vizuri katika mechi za mwanzo kuliko timu nyingine yoyote nchini kutokana na usajili kabambe wa bei mbaya pamoja na kufanya maandalizi yake nje ya nchi, imejikuta ikiambulia kutoka sare ya bila kufungana na Prisons kwenye mechi ya kwanza huku ikipokea kipigo kitakatifu cha mabao 3-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar.
Simba walitishia kujitoa katika Ligi Kuu ya Bara na pengine wahamie Zanzibar baada ya kuangushwa katika vita ya kuwagombea mabeki wawili Mbuyu Twite na Kelvin Yondani waliopewa sifa za "ukuta wa Berlin" Yanga, lakini ni safu ya ulinzi ya Wekundu wa Msimbazi inayoonekana kuwa imara zaidi kwani haijaruhusu goli.
Bahanunzi aliibuka mfungaji bora wa katika mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (kombe la Kagame) akiwa amefunga mabao sita, hadi sasa hajafunga goli, huku mfungaji bora namba mbili Kiiza aliyemaliza na magoli matano si tu kwamba hajafunga goli bali hata penati aliyopewa kupiga kwenye mechi na Mtibwa alikosa.
Wakati hayo yakiwa kwa Yanga, hali imekuwa tofauti kwa watani wao wa jadi Simba kwani beki yao iliyokuwa ikipigiwa kelele kwa muda mrefu kuwa ni mbovu haijaruhusu bao lolote kwenye mechi mbili.
Kwenye mechi ya kwanza Simba iliichapa African Lyon mabao 3-0 na nyingine ikababua JKT Ruvu mabao 2-0, hivyo licha ya kuwa kibindoni na mabao matano na kuongoza ligi, lakini pia wavu wake haujaguswa mpaka sasa.
chanzo:nipashe
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment