Yanga iliyotangulia kufungwa mabao mawili nyumbani ilicharuka na kuilaza Ruvu Shooting 3-2 katika pambano kali la kusisimua la ligi kuu ya Bara ambalo wageni walicheza vizuri mwanzoni na mwishoni mwa mchezo, jana.
Ruvu Shooting iliongoza kwa mabao mawili ndani ya dakika 10 za kwanza, lakini mabingwa wa zamani wa Bara walikusanya nguvu, Didier Kavumbagu akiifungia la ushindi katikati ya kipindi cha pili kwenye Uwanja wa Taifa, jijini.
Kavumbagu alifunga bao hilo baada ya mlinda mlango wa Ruvu na kipa wa zamani wa timu hiyo ya Jangwani Benjamin Haule kutema shuti la Haruna Niyonzima miguuni mwake.
Kwa ushindi huo Yanga imefikisha pointi 14, nne nyuma ya viongozi wa ligi kuu Simba huku timu zote mbili zikiwa zimecheza mechi nane.
Mbuyi Twite alifunga bao la kwanza la Yanga katika dakika ya 20 kwa mpira wa adhabu ndogo ambao ulikwenda moja kwa moja wavuni, kabla ya Jerry Tegete kuipatia la pili dakika ya tano tangu nusu saa ya mchezo.
Tegete alifunga goli hilo baada ya kuuwahi mpira uliowababatiza mabeki wa Ruvu; ambao ulikuwa umepigwa na Juma Abdul.
Kama bahati ingekuwa yake, Ruvu ingeweza kupata angalau sare katika mchezo huo baada ya shuti la Ernest Ernest kugonga mwamba wa juu na kutoka nje mwishoni kabisa mwa mchezo kufuatia shambulizi kali langoni mwa wenyeji.
Iliichukua Ruvu dakika mbili tu kupata bao la kwanza lililofungwa na Seif Abdallah kwa kichwa kutokana na mpira uliopigwa na Abraham Mussa.
Ilimchukua Abdallah dakika sita zaidi kufunga bao la pili la Ruvu akiunganisha mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Said Dilunga.
Kwa kipigo hicho, Ruvu inabaki na pointi tisa baada ya mechi nane pia.
Kocha wa Ruvu na mwalimu wa zamani wa Yanga Charles Boniface Mkwasa alisema timu yake ilifungwa kwa sababu wachezaji wake walibweteka baada ya kupata mabao ya mapema.
Ernie Brandts, kocha Mholanzi wa Yanga alisema mchezo ulikuwa mgumu na vijana wake walifanya kazi nzuri kupata ushindi baada ya kuwa walitangulia kufungwa.
Timu zilikuwa:
YANGA: Yaw Berko, Juma Abdul (Juma Seif dk.75), Oscar Joshua, Nadir Haroub, Mbuyu Twite, Rashid Gumbo (Haruna Shamte dk.64), Nurdin Bakari, Haruna Niyonzima, Jerry Tegete, Didier Kavumbagu, David Luhende.
RUVU: Benjamin Haule, Michael Aidan, Baraka Jaffari, George Otei, Ibrahim Shaaban, Ernest Ernest, Raphael Kyala, Hassan Dilunga.
chanzo: Nipashe
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment