Pages

Wednesday 27 February 2013

Kocha Azam afungiwa kwa kumwaga radhi dimbani


KAMATI ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imemfungia mechi tatu kocha wa Azam Fc, raia wa Uingereza Stewart Hall, sambamba na kupigwa faini ya sh 500,000 baada ya kuchojoa bukta yake wakati timu yake ilipokwaana na Kagera Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom kwenye Uwanja wa Chamazi Complex, Chamazi, jijini Dar es Salaam.
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alisema jijini Dar es Salaam jana kwamba kamati hiyo ilikutana mwishoni mwa wiki kupitia ripoti za michuano ya Ligi Kuu (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza (FDL), msimu wa 2012/2013 inayoendelea hivi sasa na kufanya uamuzi mbalimbali.
Alisema mbali ya kuvua bukta, Stewart pia alimlalamikia mwamuzi wa mechi hiyo. Vile vile Azam FC imepigwa faini ya sh 300,000 kwa kuchelewa kufika uwanjani kwenye mechi kati yake na JKT Oljoro iliyochezwa Chamazi Complex Novemba 7.
Kocha Msaidizi wa Mgambo Shooting, Denis Mwingira, naye ametozwa faini ya sh 500,000 kwa kumtolea lugha chafu mwamuzi kwenye mechi dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Manungu.
Coastal Union imepigwa faini ya sh 500,000 kutokana na mashabiki wake kumrushia chupa za maji mwamuzi msaidizi namba mbili wakati wa mechi yao dhidi ya Simba iliyochezwa Oktoba mwaka jana Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, huku African Lyon ikipata adhabu kama hiyo kwa kugoma kuingia kwenye chumba cha kubadilishia nguo wakati wa mapumziko katika mechi dhidi ya Coastal Union iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Oktoba 24, mwaka jana.
Naye kocha msaidizi wa Polisi Morogoro, Ally Jangalu, amepigwa faini ya sh 500,000 baada ya kutolewa kwenye benchi kwa kupinga uamuzi wa refa kwa sauti ya juu katika mechi kati yao na Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Novemba 10.
Wambura alisema matukio ya aina hiyo kwa kocha Jangalu, yamekuwa ya kujirudiarudia kwani Oktoba 13 mwaka jana katika mechi dhidi ya Azam mjini Morogoro, aliondolewa na mwamuzi kwenye benchi kwa kuchochea wachezaji wa timu yake wacheze rafu.
Aidha Kocha wa Moro United inayoshiriki FDL, Yusuf Macho, amepigwa faini ya sh 200,000 kwa kumtolea lugha chafu refa baada ya mechi dhidi ya Transit Camp Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi, Pwani Novemba 4 mwaka jana huku kocha wa Burkina Faso, Hasheem Mkingie, naye akilimwa faini hiyo baada ya kutolewa kwenye benchi kwa kutoa lugha chafu katika mechi ya FDL dhidi ya Mkamba Rangers.
Adhabu nyingine ni kwa kiongozi wa Majimaji, Joseph Nswila, aliyefungiwa miezi sita kwa kuingia uwanjani baada ya mechi dhidi ya Mlale JKT kumalizika na kuvamia waamuzi.
Pia kamati hiyo imemuondoa mwamuzi msaidizi anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Ferdinand Chacha, Alex Mahagi, Methusela Musebula, Lingstone Lwiza, Idd Mikongoti na Samson Kobe, kuchezesha mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara inayoendelea nchini hivi sasa, baada ya kupata alama za chini.
Waamuzi wengine wameondolewa kwa kutomudu mechi walizochezesha ambao ni Mathew Akrama, Ephraim Ndissa, Ronald Swai huku Masoud Mkelemi aliyekuwa mwamuzi wa mezani katika mechi ya FDL kati ya Moro United na Villa Squad akiondolewa kwa kutofika kwenye mkutano wa maandalizi ya mechi na alichelewa kwa dakika tano kufika uwanjani.
Katika hatua nyingine, baadhi ya makamishna wa VPL na FDL wameondolewa na wengine kusimamishwa kusimamia mechi za ligi hizo kutokana na upungufu kwenye ripoti zao au kutowasilisha kabisa ripoti hizo TFF baada ya mechi.
Hao ni Mohamed Jumbe, Hakim Byemba, Charles Komba na Mohamed Nyange.
Timu za Burkina Faso ya Morogoro, Pamba ya Mwanza Mkamba Rangers, Polisi Dodoma zimepigwa faini ya sh 200,000 kutokana na makosa mbalimbakli.
Pia klabu kadhaa zimeandikiwa barua za onyo kwa kuchelewa kufika uwanjani au kutofika kwenye mkutano wa maandalizi ya mechi nazo ni Coastal Union, JKT Ruvu, Toto Africans, Simba, Green Warriors, Majimaji, Mkamba Rangers, Polisi Dodoma, JKT Kanembwa na Moro United.
Aidha mchezaji Stanley Nkomola wa JKT Ruvu baada ya mechi dhidi ya Coastal Union, alikwenda jukwaani na kuanza kupigana na mashabiki. Pia kipa wa Transit Camp, Baltazar Makene, baada ya mechi dhidi ya Tessema aliruka uzio na kwenda kupigana na mashabiki.
Wambura alisema kwa vile masuala ya wachezaji hao ni ya kinidhamu, yamepelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu inayoongozwa na Kamishna mstaafu wa Polisi (CP), Alfred Tibaigana, kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.
source:daima

1 comment: