Pages

Tuesday 4 September 2012

Henry aonya kuhusu ufujaji pesa

Mmiliki wa klabu ya soka ya Liverpool, John Henry, amewaonya mashabiki kuhusu klabu kutumia pesa pasipo tahadhari, lakini ameelezea kwamba kama mmiliki anayajali maslahi ya klabu.

Kwa barua wazi kwa mashabiki, mmiliki mkuu John Henry aliwaandikia: "Kamwe hatutakiacha klabu katika hali hatari kama tulivyokipata tulipochukua hatamu za uongozi Anfield."

Liverpool hawajapata ushindi katika mechi zao tatu za mwanzo wa ligi, na ukiwa ndio mwanzo mbovu zaidi katika kipindi cha miaka 50. 

Henry alielezea masikitiko ya klabu kushindwa kumsajili mshambulizi mpya. 

Meneja wa Liverpool, Brendan Rodgers, amekiri kwamba kama angelijua hataweza kumsajili mshambulizi mpya kwa nia ya kuimarisha kikosi chake, basi asingemruhusu Andy Carroll kujiunga na klabu ya West Ham.


Rodgers alimuacha mshambulizi huyo wa timu ya taifa ya England kuelekea Upton Park, akiwa anaamini kwamba atafanikiwa kumkaribisha Clint Dempsey kutoka Fulham, na kumchukua mchezaji wa Chelsea, Daniel Sturridge kwa mkopo. 

Meneja huyo ana uhuru wa kumrudisha tena Carroll, aliyeondoka kwa mkopo, ifikapo mwezi Januari, na aliyehama kwa maelewano kwamba ataichezea West Ham msimu mzima.

Rodgers hata hivyo amekanusha habari kwamba alipotoshwa na matajiri wa Marekani wa klabu ya Liverpool, kampuni ya Fenway Sports Group, kuhusiana na hali ya usajili. 

Kupitia barua hiyo ambayo ilichapishwa katika wavuti rasmi ya klabu, Henri aliongezea: "Mimi kama shabiki yoyote yule wa klabu ya Liverpool nimevunjika moyo kwa kushindwa kuimarisha kikosi chetu kwa upande wa ushambulizi wakati wa dirisha la usajili msimu huu wa joto.

"Lakini hayo sio kutokana na wahusika kukosa nia wala ari ya kutofanya hivyo. 

"Walijitahidi kadri ya uwezo wao wote wakati muda wa mwisho wa usajili ulipokaribia, kwa kuwalenga washambulizi kadha waliowataka, lakini wakati huu wakashindwa kufanikiwa.

"Lakini ni kupitia msimu huu wa joto ambao wachezaji watatu wenye kipawa wamepatikana, Joe Allen, Nuri Sahin na Fabio Borini, na vijana wengine wawili wanaotazamiwa kuwika siku zijazo, Samed Yesil na Oussama Assaidi, kwa hiyo huwezi kuelezea hayo kama udhaifu katika kuimarisha timu ya siku zijazo." 

Kushindwa na Arsenal magoli 2-0 siku ya Jumapili kunamaanisha kwamba baada ya kulemewa katika mechi tatu za mwanzo, Liverpool sasa imo katika nafasi ya 18 ya ligi ya Premier. 

Henry na wawekezaji wenzake, na ambao waliichukua Liverpool mwezi Oktoba mwaka 2010, wameelezea kwamba wao wanaangazia maendeleo ya muda mrefu ya klabu, na aligusia pia juu ya mikataba mipya kwa wachezaji Daniel Agger, Martin Skrtel na Luis Suarez. 

"Hakuna yeyote anayefaa kukosa imani na juhudi zetu za kuimarisha klabu. Kupitia Brendan Rodgers, tuna meneja mwenye umri mdogo na mwenye kipawa, na ambaye tunaheshimu sana uamuzi wake kuhusiana na wachezaji na kuimarisha klabu," alielezea.
chanzo:bbc

0 comments:

Post a Comment