'Yaporwa' pesa za usajili wa Twite
Vicky Kimaro
SAKATA la Simba kumdai fedha za usajili mchezaji Mbuyu Twite limechukua mtikisiko mpya baada ya kocha wa timu ya Taifa ya Rwanda, Sredojevic Milutin 'Micho' kukata Sh20 milioni kati ya Sh30 milioni anazodaiwa mchezaji huyo ili kufidia deni lake analoidai klabu hiyo muda mrefu.
Kwa mujibu wa barua ya Micho kwenda Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), klabu ya Simba na Yanga, amekata pesa hizo kwa nguvu ili kufidia pesa ambazo Simba waliahidi kumpa alipowasaidia usajili wa mshambuliaji Felix Sunzu.
Kwa mujibu wa barua ya Micho kwenda klabu ya Simba na kopi kutumwa Yanga na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Micho amekata deni lake la Milioni 20 za Simba walizompa Twite ambazo alikuwa akizidai kwa muda mrefu.
Katika barua hiyo, Micho amesaini kupokea dola 20,000 kutoka Twite ambazo deni la wanalodaiwa Simba baada ya kukamilisha usajili wa Sunzu kutoka Al Hilal ya Sudan ambayo alikuwa akifundisha awali kabla ya kwenda Rwanda.
"Julai 2011, niliidhamini Simba ili kumsajili Sunzu, lakini tofauti na makubaliano hawakulipa fedha hizo za usajili na mimi nilikatwa mshahara na klabu yangu ili kufidia deni hilo" alisema Micho katika barua hiyo.
Aliongeza: "Baada ya kufanya mazungumzo mara kwa mara na Makamu Mwenyekiti Simba, Geofrey Nyange 'Kaburu' hakuna kilichotekelezwa zaidi ya ahadi hewana kunipa ahadi hewa.
"Uongozi wa juu wa Simba unajua kila kitu kuhusu suala hili hata Rais wa TFF, Leodegar Tenga na aliyekuwa Makamu wa Rais Cresentius Magori wanafahamu deni langu kwa Simba.
"Sina namna ya kulipwa pesa hizo, hivyo nimeamua mwenyewe kuchukua kwa nguvu pesa anazodaiwa Twite ili kufidia deni langi," aliongeza Micho.
Akijibu madai hayo ya Kaburu alisema ni kweli Micho alisaidia kufanikisha usajili wa Sunzu, lakini hakukuwa na makubaliano ya maandishi juu ya malipo ya fedha hizo.
"Siwezi kukana kwamba Micho alitusaidia, lakini kama kulikuwa na malipo yoyote kwa Al Hilal walipaswa kutuambia na sisi kulipa fedha hizo, siyo hiki anachosema yeye."
Naye Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alipoulizwa juu ya suala hilo alisema: "Hatutaki mshenga wala mjumbe, pesa tulimpa mkononi zikiwa kamili na tunamtaka azirejeshe kama zilivyokuwa."
Kauli ya Micho imekuja wakati Simba wameshatishia kumfikisha Twite mahakamani kwa madai ya kuwatapeli milioni 30 za usajili alizopewa na mwenyekiti wao Ismail Aden Rage.
Mwanzoni mwa wiki hii, Mwenyekiti wa kundi la Marafiki wa Simba, Zakaria Hanspop alisema walipanga kukutana na Yanga kujadili suala la Twite, lakini wapinzani wao hawakutokea.
"Wiki hii tulikuwa tukutane na Yanga ili tumalizane lakini hawajatokea, hatuna sana na shida ya Sh30 milioni. Twite ataitwa mahakamani muda wowote kujibu kesi ya utapeli," alisema Hanspop.
chanzo:http://www.mwananchi.co.tz
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment