Pages

Wednesday, 5 September 2012

ZAHARAN AONDOKA MIKONO MITUPU LONDON!!!

MWAKILISHI wa Tanzania kwenye michezo ya Paralimpiki, Zaharan Mwenemti ameaga rasmi michuano hiyo baada ya jana mchana kushindwa kung'ara kwenye fainali ya kutupa tufe kwa walemavu wa daraja F 57/58.

Katika fainali hiyo, Zaharan amekamata nafasi ya 16 kati ya washiriki 18 akiwa ametupa umbali wa mita 9 na setimita 52 na kujinyakulia pointi 403 ikiwa ni mchezo wake wa pili kufanya vibaya kwenye michuano hiyo.

Awali mwakilishi huyo pekee wa Tanzania alikamata nafasi kama hiyo kwenye fainali ya kutupa kisahani wiki iliyopita,ambayo iliyofanyika kwenye Uwanja wa Olympic jijini London.

Russia ndiyo imekuwa kinara baada ya Ashapatov Alexey kutupa umbali wa mita 16 na sentimita 20 na kujinyakulia medali ya dhahabu akiwa na pointi 989.

Nafasi ya pili ilikwenda kwa Rokicki Janusz wa Poland aliyetupa umbali wa mita 15 na sentimita 68 na kutwaa Medali ya Fedha akiwa na pointi 960 huku Louwrens.

Michael wa Afrika Kusini akifunga pazia la ushindi kwa kutwaa Medali ya Shaba akiwa ametupa umbali wa mita 13 na CM 64 akiwa na pointi 958.

Wachezaji Kponhinto Constant wa Benin iliyokamata nafasi ya 17 na Bilal Sidi Mohamed wa Maurtania aliyeshika mkia ndiyo walikuwa vibonde wa Zaharan kwenye michuano hiyo itakayofikia tamati Septemba 9.

Kwa matokeo hayo Zaharan ameendeleza rekodi ya Tanzania kufanya vibaya jijini London baada ya mwezi uliopita wachezaji wa ngumi, riadha na kuogelea kutoka kapa kwenye michezo ya Olimpiki.
chanzo:http://www.mwananchi.co.tz

0 comments:

Post a Comment