Pages

Monday, 24 September 2012

SIMBA YA NGURUMA KILELENI!!

Simba iliendeleza ushindi wa asilimia 100 baada ya kuifunga Ruvu Shooting 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salam na kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Magoli kutoka kwa Mzambia Felix Sunzu na yosso anayeinukia Edward Christopher yaliwapa mabingwa ushindi wa tatu mfululizo uliofanya wafikishe pointi 9, mbili juu ya washindi wa pili wa msimu uliopita, Azam, walio katika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 7. Nafasi ya tatu inashikwa na Tanzania Prisons ambao jana walishinda 2-1 dhidi ya African Lyon kwenye Uwanja wa Chamazi.

Wageni wa ligi, Mgambo JKT walibaki kuwa timu pekee ambayo haina pointi hadi sasa baada ya jana kukumbana  kipigo cha 1-0 nyumbani Mkwakwani, Tanga kutoka Kagera Sugar, kikiwa ni kipigo cha tatu mfululizo tangu walipopanda daraja.

Miamba wa soka nchini Yanga wako katika nafasi ya saba wakiwa na pointi 4, tano nyuma ya mahasimu wao Simba, baada ya juzi kufufuka katika mwanzo mbaya wa msimu na kutoa kisago cha magoli 4-1 kwa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa.  

Simba, hata hivyo, jana walihitaji goli la “usiku” kutoka kwa Eddo aliyemalizia pasi ya Mrisho Ngassa katika dakika ya 85 ili kupata ushindi katika mechi iliyoonekana kama ingemalizika kwa sare baada ya Seif Rashid kuisawazishia Ruvu Shootings katika dakika ya 75.

Rashid alisawazisha goli la kichwa la Sunzu la dakika ya 29, baada ya kumpokonya mpira beki Juma Nyosso na kupiga shuti lililomshinda kipa Juma Kaseja. 

Simba ingeweza kupata ushindi mnono zaidi wakati ilipopata penalti katika dakika ya 45, lakini mpigaji anayeaminika Daniel Akuffor alishindwa kufunga baada ya kipa Benjamin Haule kuipangua. Penalti hiyo ilitolewa na mwamuzi Ronald Swai kutoka Arusha baada ya beki wa Ruvu kuunawa mpira ndani ya boksi.
chanzo:nipashe

Baada ya mechi hiyo, kocha wa Shooting, Boniface Mkwasa alisema wachezaji wake walipoteza umakini dakika za mwisho na imekuwa kawaida kuelemewa wakati wa dakika za mwisho.

Vikosi vilikuwa Simba: Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Shomar Kapombe, Juma Nyosso, Amir Kiemba/Komalmbil Keita (dk. 88), Mwinyi Kazimoto, Ramadhani Chombo ‘Redondo’/Haruna Moshi ‘Boban’ (dk. 65), Felix Sunzu, Daniel Akuffor/Edward Christopher (dk. 65) na Mrisho Ngassa.

Ruvu Shooting: Benjamin Haule, Michael Pius, Mau Bofu, George Michael, Said Suzan, Gideon David, Abdulrahaman Mussa, Hassan Dilunga, Paul Ndauka/ Self Rashid (dk. 57),, Hussein Said na Said Dilunga
Chanzo:nipashe

0 comments:

Post a Comment