Mghana Daniel Akuffor ambaye alichukuliwa katika dakika za mwisho za dirisha la usajili lililopita, na ambaye anaelekea kuwa mtambo mpya wa mabao wa Simba jana aliwahakikishia mabingwa watetezi hao ushindi wa mechi ya kwanza ya msimu mpya wa ligi kuu ya Bara kwa bao maridadi la matomeo ya 3-0 dhidi ya African Lyon kwenye Uwanja wa Taifa.
Emmanuel Okwi alifunga goli la kwanza baada ya nusu saa ya mchezo baada ya kuwatoka mabeki wa African Lyon na kumfunga kirahisi mlinda mlango Abdul Seif.
Nossor Masoud 'Cholo' alitumia vizuri pasi ya Mrisho Ngasa kufunga bao la pili muda mfupi baadaye kuipa Simba utawala wa mchezo huo.
Lakini ni Akuffor aliyeihakikishia Simba pointi tatu kwa penalti ya katikati ya kipindi cha pili, iliyotolewa na muamuzi Owden Mbaga baada ya mkongwe Semmy Kessy kumuangusha Okwi ndani ya eneo la hatari.
Kama ilivyo katika siku ya kufa nyani, African Lyon ilipoteza nafasi nzuri ya kupata angalau bao la kujipooza baada ya Sunday Bakari kukosa penalti katika kipindi cha pili, shuti lake lilipogonga mwamba.
Penalti hiyo ilitolewa na muamuzi Mbaga baada ya kiungo wa Simba Mwinyi Kazimoto kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.
Timu zilikuwa:
Simba: Juma Kaseja, Nassor Masoud, Amir Mafta, Juma Nyoso, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba, Haruna Moshi (Salim Kinje), Daniel Akuffor, Mrisho Ngasa, Emmanuel Okwi.
African Lyon: Abdul Seif, Johannes, Hamadi Banzi, Sunday Bakari, Benedicto Mwamlanga, Sunday Hinju, Obina Salamusasa, Semmy Kessy, Idd Mbaga, Jacob Masawe, Yusuf Mpilipili.
Kutoka Morogoro, Idda Mushi anaripoti majirani Polisi Morogoro na Mtibwa Sugar jana walitoka sare ya bila magoli katika mchezo mwingine wa ligi kuu ya Bara, kwenye Uwanja wa Jamhuri.
Kocha wa Polisi John Simkoko alisema timu yake ilikosa mabao kutokana na wachezaji wake kuwa wasiwasi wa mchezo wa kwanza wa ligi lakini atajaribu kurekebisha kasoro hiyo mazoezini.
Aidha, Simkoko alimsifu kocha wa Mtibwa Sugar kwa kusema ingawa aliwahi kumfundisha kama mchezaji sasa ni mwalimu mzuri.
chanzo:Nipashe
Sunday, 16 September 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment