Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara hatua ya raundi ya pili inatarajia kuendelea leo katika viwanja saba tofauti nchini ambapo JKT Ruvu ya Pwani atawakaribisha mabingwa watetezi wa ligi hiyo Simba kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku Mtibwa Sugar nayo ikiwavaa Yanga kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
Simba itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kuanza vyema katika ligi hiyo kwa ushindi wa magoli 3-0 iliopata dhidi ya African Lyon wakati mabingwa wa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) Yanga wana pointi moja iliyotokana na suluhu dhidi ya Prisons mkoani Mbeya.
Kocha wa Simba, Milovan Cirkovic aliiambia NIPASHE kuwa kikosi chake kiko tayari kwa mchezo huo na anachotaka kuona wanapata pointi tatu.
Cirkovic alisema kurejea kwa mshambuliaji wake Mzambia Felix Sunzu kumekifanya kikosi hicho kuwa na ushindani zaidi wa namba katika eneo la ushambuliaji kutokana na kila mmoja kuonyesha kiwango cha juu mazoezini.
"Hakuna mechi nyepesi, ninachohitaji ni kuona tunashinda na kupata pointi tatu katika mechi hizi za kwanza ili kuondoa wasiwasi katika mechi za mwishoni mwa ligi, kikosi changu kimekamilika," alisema kocha huyo raia wa Serbia.
Charles Kilinda, kocha wa JKT Ruvu, aliliambia gazeti hili kuwa timu yake imejiandaa vyema na mechi zote za ligi na si kwa ajili ya kuikabili Simba tu.
Kilinda alisema kwamba anafahamu mchezo huo utakuwa na ushindani huku akisikitika kumkosa mshambuliaji wake mpya, Mussa Hassan 'Mgosi' ambaye hajapata kibali chake cha Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kutoka katika timu ya DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambayo ameichezea msimu mmoja uliopita.
Akiondoka bila ya mshambuliaji, Jerry Tegete na Rashid Gumbo, kocha wa Yanga, Tom Saintfiet, alisema kwamba mchezo wa leo dhidi ya Mtibwa Sugar utakuwa na upinzani mkubwa.
Hata hivyo, Saintfiet aliahidi kupata matokeo mazuri katika mchezo huo na kurejesha furaha kwa mashabiki wa Yanga.
"Sikufurahishwa na matokeo ya sare kule Mbeya, naahidi tutashinda mechi dhidi ya Mtibwa Sugar ingawa haitakuwa rahisi na tunaendelea kucheza kwenye uwanja usiokuwa na ubora," alisema kocha huyo.
Kocha huyo amemjumuisha kiungo wa kimataifa kutoka Rwanda, Haruna Niyonzima licha ya kuwa mgonjwa.
Kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky Maxime aliliambia gazeti hili kwamba wachezaji wake wamejiandaa vyema kushinda na hatimaye kutorudia makosa yaliyojitokea wakati wanaivaa Polisi Morogoro katika mechi ya kwanza ya ligi iliyoisha kwa sare ya 0-0 pia.
"Tuko fiti na tayari kwa mchezo, hivi (jana mchana) ndio tunaelekea Morogoro mjini kuwasubiri Yanga, naamini tutapata matokeo mazuri, tutaiangusha tu, waache waje na wachezaji wao wenye majina makubwa," Maxime aliongeza.
Mechi nyingine za ligi hiyo zitakazochezwa leo ni kati ya African Lyon dhidi ya Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Azam (Chamazi) jijini wakati Ruvu Shooting itashuka kwenye Uwanja wake wa Mabatini, Mlandizi kuikabili Mgambo Shooting kutoka Handeni, Tanga na Prisons itakuwa kwenye Uwanja wake wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya kuisubiri Coastal Union ya Tanga.
JKT Oljoro ya Arusha itaivaa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza wenyeji Toto Africans wataikaribisha Azam ambayo nayo ilianza kwa kuchukua pointi tatu ugenini Kagera.
chanzo:Nipashe
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment