Wachezaji wawili wa timu ya Yanga na timu ya Taifa Tanzania (Taifa Stars) mlinzi wa kati wa Kelvin Yondani na mshambuliaji Said Bahanunzi leo wameanza rasmi mazoezi katika Uwanja wa shule ya Sekondari Loyola kufuatia kukaa nje kwa zaidi ya wiki moja kutokana na kuwa majeruhi.
Kelvin Yondani ameanza mazoezi leo asubuhi kufuatia kuwa nje ya uwanja takribani kwa wiki mbili kufuatia kuumizwa na mchezaji Haruna Moshi 'Boban' katika mchezo wa ligi kuu ya vodacom Tanzania bara, uliowakutanisha watani wa jadi Yanga na Simba, mchezo ulioishia kwa sare ya mabao 1-1.
Katika mchezo huo Boban hakuonyesha uungwana kwa kwenda kumkanyaga Yondani hali iliyopelekea mchezaji huyo kutolewa nje ya uwanja na kushindwa kuendelea tena na mchezo, ambapo uchunguzi wa awali ulionyesha kuwa amepata mshituko katika mfupa wake mkubwa wa mguu.
Daktari wa timu ya Yanga, Dk Suphian Juma amesema, mara baada ya kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kitengo cha mifupa MOI, Yondani ameendelea kuimarika na kupata nafuu kwa haraka, hivyo leo ameanza mazoezi mepesi kujiandaa kurudi uwanjani katika michezo inayofuata.
Naye mshambuliaji Said Bhanaunzi amabye alipatwa na matatizo ya kuchanika nyama ya paja mwishoni mwa wiki iliyopita katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar mjini Bukoba, anaendelea vizuri ambapo naye siku ya leo ameanza mazoezi mepesi na Yondani chini ya uangalizi wa Daktari Suphian Juma.
Kutokana na kurejea kwa wachezaji hawa wawili, timu ya Yanga kwa sasa haina mchezaji yoyote majeruhi hivyo kocha mkuu Ernie Brandts atapata nafasi ya kumtumia mchezaji yoyote atakayemtaka katika michezo ya ligi kuu ya Vodacom inayofuata.
Yanga itashuka dimbani siku ya Jumamosi kucheza na timu ya Ruvu Shooting katika muendelezo wa ligi kuu ya Vodacom Tanzania bara.
chanzo:http://www.globalpublishers.info
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment