Pages

Saturday, 2 March 2013

Hakuna dalili uwanja wa Yanga


Hakuna dalili za kuanza kwa ujenzi wa uwanja wa kisasa wa soka wa klabu ya Yanga ifikapo Mei mwaka huu kama ilivyoahidiwa, baada ya uongozi kushindwa kuanza kukusanya fedha kwa ajili ya shughuli hiyo mpaka sasa.
 
Uongozi wa mabingwa hao wa soka Afrika Mashariki na Kati uliahidi kuanza kujenga uwanja wa kisasa wenye uwezo wa kuketisha watazamaji 40,000 katika mkutano mkuu wa wanachama wa Yanga uliofanyika jijini Dar es Salaam Januari 20 mwaka huu.
 
Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga alisema wameshaingia mkataba wa makubaliano ya kujenga uwanja huo na kampuni ya Beijing Constructions Engineering ya China iliyojenga Uwanja wa Taifa na kuendelea kufanyia ukarabati Uwanja wa Uhuru jijini.
 
Akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Afisa Habari wa klabu hiyo, Baraka Kizuguto alisema kuwa uongozi wa Yanga bado haujaanza kukusanya fedha za ujenzi wa uwanja huo lakini “zoezi hilo litaanza kufanyika muda wowote.”
 
Alisema kuwa uongozi unajipanga kuanza kusaka fedha hizo ili kazi hiyo ianze kufanyika Mei kama ulivyoahidi.
 
“Bado hatuajaanza kukusanya fedha. Tutawataarifu mipango itakavyokuwa imekamilika,” alisema Kizuguto ambaye alipewa kazi hiyo baada ya kusimamishwa kazi kwa aliyekuwa Afisa Habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu mwishoni mwa mwaka jana.
 
Mbinu zilizopendekezwa na uongozi wa Yanga kukusanya kiasi cha Sh. bilioni 32 ni pamoja na kufanya harambee na michango ya wanachama wa klabu hiyo.
 
Wakati huo huo, mechi ya ligi kuu ya Bara kati ya Yanga na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa jijini Jumatano ambayo ilishuhudiwa na mashabiki 13,398 waliokata tiketi imeingiza Sh. milioni 77. 
 
Kwa mujibu wa Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, kila klabu ilipata mgawo wa Sh. milioni 18.2.
 
Yanga wanaongoza msimamo wa ligi hiyo wakiwa na pointi 42 baada ya mechi 18 wakifuatiwa na mabingwa wa Kombe la Mapinduzi, Azam FC (36) na mabingwa watetezi Simba (31).
chanzo:nipashe

0 comments:

Post a Comment