Pages

Sunday 3 March 2013

Simba mwaka wa taabu, Azam FC yafanya kweli


TIMU ya Simba, jana, iliaga michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa mabao na Libolo ya Angola katika mechi ya marudiano ya hatua ya awali ya michuano hiyo yenye utajiri mkubwa kwa ngazi ya klabu.
Kwa kipigo hicho, Simba chini ya kocha wake Mholanzi, Patrick Liewig, wameaga kwa kulimwa jumla ya mabao 5-0.
Katika mechi ya kwanza iliyopigwa wiki mbili zilizopita Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, walifungwa bao 1-0.
Hata hivyo, dalili za kung’olewa mapema kwa Simba iliyowahi kufika hatua ya nane bora ya michuano hiyo mwaka 2003, zilionekana mapema kwa kuonyesha kiwango butu chini ya Liewig aliyeitwaa timu hiyo Novemba mwaka jana kutoka kwa Mserbia, Milovan Cirkovic.
Wakati Simba ikiangukia pua, wawakilishi wengine kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho, Azam FC, wameitoa Tanzania kimasomaso kwa kutinga raundi ya kwanza baada ya kuwang’oa Al Nasr Juba ya Sudan Kusini. Baada ya kushinda mabao 3-1 katika mechi ya kwanza kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, Azam jana walidhihirisha ubora wao kwa kuwafunga wapinzani wao 5-0, hivyo kusonga mbele kwa jumla ya mabao 8-1.
Wafungaji kwa upande wa Azam katika mechi ya jana iliyochezwa mjini Juba, ni John Bocco aliyefunga mabao mawili na Hamis Mcha naye aliyefunga mawili huku moja likifungwa na Kipre Tchetche, nyota wa kimataifa wa Ivory Coast.
Matokeo hayo ni faraja kubwa kwa wachezaji, viongozi, wapenzi na mashabiki wa timu hiyo ambayo ni mara ya kwanza kwao kushiriki michuano ya kimataifa tangu kuanzishwa kwao Juni 24, mwaka 2007.
Azam waliipata nafasi hiyo baada ya kumaliza nafasi ya pili katika msimu uliopita nyuma ya Simba iliyokuwa bingwa huku Yanga ikiwa ya tatu, hivyo kukosa tiketi ya kucheza michuano ya kimataifa.
chanzo:Daima

0 comments:

Post a Comment