MABINGWA mara 23 wa Tanzania bara tangu mwaka 1965, Yanga, jana walizidi kujisafishia njia kuelekea ubingwa msimu huu baada ya kuwanyuka Toto African bao 1-0.
Kwa ushindi huo, Yanga chini ya Kocha Ernie Brandts wamefikisha pointi 45, hivyo kuzidi kukalia uongozi wa ligi ikifuatiwa kwa karibu na Azam yenye pointi 37.
Yanga walianza kulikaribia lango la ndugu zao Toto dakika ya 37, lakini Jerry Tegete, mtoto wa Meneja wa Uwanja wa CCM Kirumba, akashindwa kuitumia vizuri nafasi hiyo.
Kabla ya hapo, dakika ya 33 Erick Mlilo wa Toto alilimwa kadi ya njano na mwamuzi Endrew Shamba wa Pwani kwa mchezo mbaya.
Dakika ya 44, Emmanuel Swita pia wa Toto alilimwa kadi ya njano kwa mchezo mbaya.
Hadi mapumziko hakuna timu iliyokuwa imepata bao licha ya kuwepo kwa mashambulizi makali kwa timu zote.
Yanga walikianza kipindi cha pili kwa mashambulizi makali, lakini mabeki wa Toto walikuwa makini kuokoa hatari.
Dakika ya 47 na 53, Simon Msuva alipata nafasi ya kufunga kutokana na kazi nzuri ya Hamis Kiiza, lakini alishindwa kufanya hivyo.
Toto walimtoa Mohamed Jinga na kuingia Hery Mohamed dakika ya 63, pia wakamtoa Selemani Kibuta na kuingia Chika Oulge.
Dakika ya 68, Mlilo alilimwa kadi ya njano kwa kumchezea vibaya Msuva.
Yanga walimtoa Tegete dakika ya 74 na kuingia Nizar Khalfan ambaye dakika nne baadae aliifungia timu yake bao hilo pekee kwa kichwa akiunganisha krosi maridadi ya Kiiza.
Dakika ya 83, Kiiza alikosa bao baada ya shuti yake kupaa juu ya lango kabla ya Msuva naye kushindwa kufunga dakika ya 86.
Yanga wanapaswa kujilaumu wenyewe kwa kushindwa kuzitumia nafasi walizopata.
Wakati Yanga ikizidi kupasua anga kuelekea ubingwa, washindani wao wa karibu, Azam jana walivutwa shati na Polisi Moro kwa kutoka sare ya bao 1-1 Uwanja wa Chamazi.
Matokeo hayo yameipa Yanga nafasi ya kuongoza kwa tofauti kubwa ya pointi nane, kwani wakati Azam ikifikisha pointi 37, Yanga inatanua kileleni kwa pointi 45.
Yanga: Ally Musa, Godfrey Taita, David Luhende, Mbuyu Twite, Kelvin Yondan, Athuman Idd ‘Chuji,’ Simon Msuva, Frank Domayo, Jerry Tegete/Nizar Khalfan, Hamis Kiiza na Haruna Niyonzima.
Toto: Erick Ngwege, Erick Mlilo, Robert Magadula, Erick Kyaruzi, Everist Maganga, Hamis Msafiri, Severine Constatine, Emmanuel Swita, Chika Olugbe, Musa Musa/Simba Boaz na Mohamed Jinga/Hery Mohamed.

chanzo:daima
0 comments:
Post a Comment